Mwenyekiti mtendaji wa IPP DR. REGINALD MENGI ameeleza kushtushwa na taarifa zilizochapishwa kwenye gazeti la TAIFA IMARA zikimtuhumu kuwa ana nia ya kutaka kuiangusha serikali ya Rais Kikwete na kumshughulikia baada ya kumaliza muda wake wa uongozi, kunyamaziwa na ikulu na idara ya habari maelezo kwa wiki tatu bila kutoa ufafanuzi wowote.
Katika kauli yake kwa vyombo vya habari Dr. Mengi amesema taarifa hiyo ya Gazeti hilo iliyochapishwa Machi 23 2015 ilikuwa na kichwa cha habari kinachosema "ZITTO KABWE AMCHONGEA MENGI KWA RAISI JAKAYA KIKWETE..." ambayo pia imesema Rais Kikwete aliapa kupambana naye inampa hofu kubwa kuhusu mustakabali wa maisha yake kutokana na kuachwa kuendelea kusambaa kwa tuhuma hizo bila kukanushwa au kuzitolea maelezo yoyote kwa wiki tatu sasa.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Dr. Mengi amesema taarifa hiyo ambayo chanzo chake ni ikulu ya Tanzania, inasema kwamba Zitto Kabwe alimpelekea raisi Kikwete taarifa kwamba yeye (Mengi) ndio kinara wa kuhujumu serikali yake na muda mfupi tu mara baada ya Zitto Kabwe kuwasilisha bungeni taarifa ya kamati ya kudumu ya Bunge ya hesabu za serikali kuhusu kashfa ya Tegeta-ESCROW ambayo yeye (Zitto) alikuwa mwenyekiti wake.
Sehemu ya taarifa hiyo ya Dk. Mengi kwa vyombo vya habari inasema:
"Katika habari hiyo inasema Zitto amekwenda mbali zaidi kwa kumwambia raisi Kikwete kuwa Dk. Mengi ameapa kuwa raisi Kikwete akimaliza muda wake wa uraisi atamshughulikia kwa nguvu zake zote. Habari hiyo imeeleza kwamba baada ya maelezo hayo raisi Kikwete aliapa kupambana na Dk. Mengi na akamshuru sana Zitto kwa kumpa taarifa hizo.
Kauli yangu:
Tuhuma zilizotolewa kuhusu nia yangu ya kutaka kuiangusha serikali ya raisi Kikwete na kumshughulikia baada ya kumaliza muda wake wa uongozi zimenishtua sana, na tamko kwamba raisi Kikwete ameapa kuwa atapambana na mimi, imenipa hofu kubwa kuhusu mustakabali wa maisha yangu. Hofu yangu kubwa inasababishwa na Ikulu na Idara ya habari maelezo kukaa kimya kwa zaidi ya wiki tatu biila kutoa ufafanuzi wowote. Najua umakini wa kurugenzi ya mawasiliano ikulu na idara ya habari maelezo katika kutoa ufafanuzi wa haraka wa jambo lolote linalomhusu raisi. Lakini katika hili nashangaa kuona taasisi hizo zimeamua kukaa kimya na kuacha tuhuma hizo kusambaa."
Dk. amesema ukubwa wa hofu hiyo ni kutokana na Raisi ambaye ni mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama kauli yake kama ilivyonukuliwa na Gazeti kuwa atapambana naye inaweza kuchukuliwa kama agizo kwa vyombo vya dola kumuangamiza.
"Hofu yangu inazidi kuwa kubwa sana kwa sababu, raisi ni mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama. Kauli yake kama ilivyonukuliwa na gazeti hilo kwamba atapambana na mimi inaweza kuchukuliwa kama agizo kwa vyombo vya dola viniangaminize. Kwa mfano mwaka 1170, akofu mkuu wa Canterbury nchini Uingereza aliuawa baada ya walinzi wa mfalme kusikia mfalme akisema, namnukuu "hakuna anayeweza kuniondolea huyu Mturuki?" mwisho wa kunukuu. Walinzi wake wakadhani mfalme ameagiza wamuue askofu huyo, na wakamuua", ilisema taarifa hiyo ya Dk. Mengi.
No comments:
Post a Comment
TUNAOMBA MAONI YAKO JUU YA HII HABARI HAPA CHINI