,,,,

bar

Friday, 17 April 2015

Waziri Sitta awafukuza vigogo wa kampuni ya reli nchini (TRL)..... Madeni Kipande Wa TPA amefukuzwa kazi rasmi


SERIKALI imewasimamisha kazi karibu viongozi wote wakuu wa Kampuni ya Reli nchini (TRL), kwa kile kilichoelezwa kuwa hujuma ya mabilioni ya shilingi yaliyotumika kununua mabehewa chakavu.

Waliosimamishwa ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji, Kipallo Kisamfu, Mhandisi Mkuu wa Mitambo, Ngosomwile Ngosomiles, Mhasibu Mkuu, Mbaraka Mchopa, Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Jasper Kisiraga na Meneja Mkuu wa Manunuzi wa kampuni hiyo, Ferdinand Soka.
 
Wakati hayo yakiwakuta hao, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Madeni Kipande aliyekuwa amesimamishwa kazi kutokana na tuhuma mbalimbali, sasa amefukuzwa rasmi.
 
Hayo yaliwekwa hadharani jana na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta alipokutana na waandishi wa habari na kutoa taarifa ya uchunguzi kuhusu ununuzi wa mabehewa machavu katika Kampuni ya Reli nchini.
 
Sitta, mmoja wa wanasiasa wakongwe aliyeshika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwa ni pamoja na uwaziri tangu enzi za utawala wa Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Julius K. Nyerere, alisema mbali ya madudu yaliyoonekana katika kamati iliyoundwa na mtangulizi wake katika wizara hiyo, Dk Harrison Mwakyembe, waligundua mambo mengi Jumatatu wiki hii.
 
Yaliyogunduliwa ni pamoja na ukiukwaji mkubwa wa masharti ya mkataba wa ununuzi wa mabehewa hayo, kwani mzabuni alilipwa fedha zote, tofauti na taarifa za awali iliyoonesha malipo yangefanyika kwa awamu.
 
“Hivyo wizara ina maoni kwamba mazingira ya utekelezaji wa mkataba huu yana dalili za hujuma kwa TRL na kwa nchi yetu na siyo uzembe,” alisema Sitta. 
 
Akifafanua hilo alisema TRL iliagiza mabehewa ya mizigo 274 ambapo zabuni ilikwenda kwa Kampuni ya Hindustan & Industrial Engineering Limited ya India, ambapo katika uagizwaji wa mabehewa hayo kulikuwa na uzembe katika ufuatiliaji kiwandani, pamoja na uzembe katika kuyapokea yakiwa mabovu.
 
  • Alisema mabehewa hayo yalipofikia 150 aliyazuiya, hivyo 124 yakawa bado hayajafika nchini. Sitta alisema kwa mujibu wa taarifa alizonazo ilibidi mpaka sasa asilimia 50 ya gharama ya mabehewa hayo iwe imeshalipwa, lakini kinyume chake nyaraka zinaonyesha mpaka sasa pamoja na kuzuiwa kwa mabehewa 124 mzabuni huyo ameshalipwa asilimia 100.
 
“Huu ni uzembe, ni hujuma kama kiongozi sitamstahi yeyote atakayekuwa sehemu ya hujuma,” alisema Sitta.
 
Alisema kutokana na hali hiyo ameagiza kwamba uchunguzi wa kubaini uwezekano wa hujuma ufanyike, hivyo amemwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka asimamie kuundwa kwa kamati ya uchunguzi.
 
Alisema kamati hiyo itaongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi katika Sekta ya Umma (PPRA), na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
 
Sitta ametoa wiki tatu kuanzia Jumatatu ijayo Aprili 20, mwaka huu kuchunguza na kukamilisha kazi. Katika kipindi hicho, viongozi wakuu wa kampuni hiyo ya reli wanaowajibika na mkondo wa kashfa hiyo ya uagizaji na malipo ya ununuzi wa mabehewa hayo wote wamesimamishwa kupisha uchunguzi huo.
 
Aidha, alisema tangu mwanzoni mwa mwaka huu serikali ilikuwa ikifanyia kazi tuhuma zinazohusu mabehewa mabovu ya mizigo yaliyoagizwa kutoka India na TRL, baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa tuhuma hizo na kamati iliyoundwa na Mwakyembe, aliagiza bodi ya wakurugenzi ya TRL ipitie taarifa hiyo na maelezo ya suala zima la mabehewa hayo.
 
Alisema katika uchunguzi huo ilibainika kuwa mabehewa mengi kati ya yaliyoagizwa yana kasoro, pia kulikuwa na uzembe katika uagizaji na ufuatiliaji kiwandani yalipokuwa yanatengenezwa na kulikuwa na uzembe katika kuendelea kuyapokea mabehewa hayo pamoja na ubovu wake kujulikana.
 
Alisema amemteua Elias Mshana kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji hadi hapo uchunguzi utakapokamilika. Pia ameagiza bodi ya wakurugenzi ya TRL ikutane kuteua watumishi wenye sifa kukaimu nafasi wanaozishikilia waliosimamishwa kazi.
 
Kipande wa TPA  Akizungumza suala la Kipande, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari aliyekuwa amesimamishwa kazi tangu Februari 16, mwaka huu ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali dhidi yake, Sitta alisema Tume aliyoichagua ilikamilisha kazi yake Machi 20, na kumkabidhi taarifa ya uchunguzi wao Machi 24 kwa hatua zaidi.
 
“Baada ya kuisoma taarifa ya tume na hatimaye kushauriana na taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala haya, tumeridhika pasipo mashaka yoyote kwamba isingefaa Madeni Kipande kuendelea na kazi ya kuongoza Mamlaka ya Bandari.
 
“Hii ni kutokana na kuridhika na utawala mbovu aliouendesha uliosababisha manung’uniko mengi miongoni mwa wateja na wadau wa bandari na mgawanyiko mkubwa wa wafanyakazi,” alisema Sitta. 
 
Alisema kutokana na hali hiyo, serikali imeamua kumrejesha Kipande Idara Kuu ya Utumishi ili aweze kupangiwa majukumu mengine.
 
“Kipande ameonekana hafai kuongoza bandari ana maamuzi ya pupa, yasiyofuata taratibu pia yenye karaha. Tulichunguza uwezo wake wa kuendesha mamlaka ya bandari sasa kishapwaya inabidi arudishwe utumishi.
 
Hapa hatujachunguza masuala ya jinai, bali uwezo wa kutenda kazi,” alisema Sitta.
 
Tangu kusimamishwa kwa Kipande ambaye alikuwa anakaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu, Ephraim Mgawe aliyekuwa ameondolewa kutokana na tuhuma mbalimbali, nafasi hiyo sasa inashikiliwa na Awadhi Massawe aliyepata baraka za Waziri Sitta na kuendelea kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu TPA.

1 comment:

  1. Hii nchi yetu nahisi imelaaniwa, kwa nini kila kona ni wizi? Popote linapotokea jambo la maana na la msingi, lazima wezi pia wapo. Tunahitaji mkono wa Mungu kujinasua katika jinamizi hili, la sivyo tutaogopwa.

    ReplyDelete

TUNAOMBA MAONI YAKO JUU YA HII HABARI HAPA CHINI

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Labels

Afya (4) Habari (37) Magazeti (11) Michezo (8) Picha zinazungumza. (6) Sheria (1) Siasa (10) Uhusiano (2)