RAIS Jakaya Kikwete ameahidi kuongeza mishahara ya wafanyakazi kuanzia Julai mwaka huu, ili walau kima cha chini kikaribie Sh 315,000 ambazo Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) limekuwa likiipigia kelele kwa muda mrefu.
Kikwete alisema hayo alipokuwa akihutubia wananchi waliohudhuria sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani, zilizofanyika kitaifa kwenye viwanja vya CCM Kirumba jijini Mwanza jana.
Rais Kikwete alisema, “Ongezeko lililoko ni dogo sana lakini si haba. Na mwaka huu tutaongeza mshahara kufikia Sh 315,000 kima cha chini na kama hakitafikia, tutaangalia mahesabu yetu kwa nini, angalau ikaribie hiyo”.
Rais Kikwete alisema serikali imechukua hatua za makusudi za kuongeza mshahara kila mwaka tangu alipoingia madarakani mwaka 2005 ambapo kima cha chini alikuta Sh 65,000 na amekipandisha na sasa kimefika Sh 265,000 ambayo ni zaidi ya mara nne.
Kuhusu kauli iliyotolewa na vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa kuwa serikali imepanga kusogeza uchaguzi mkuu usifanyike Oktoba mwaka huu ili kumuongezea muda Rais Kikwete aendelee kutawala, amejibu na kusema hana mpango huo.
“Nimesikia wazee (viongozi wa Ukawa) wanasema serikali haina mpango wa kufanya uchaguzi. Urais wangu hauna mpango wa kufanya hivyo. Aibu! Sijui maneno haya wameyatoa wapi...” alisema.
Kwa upande mwingine alisema serikali imeendelea kupunguza kiwango cha kodi wanayotozwa wafanyakazi (PAYE) mwaka hadi mwaka. Alikuta asilimia 18.5 na kimeshuka katika utawala wake na kufikia asilimia 12.
“Na mwaka huu tutapunguza sijui tutafikia asilimia 9 kama mnavyotaka ila tutakapofikia si pabaya,” alisema Kikwete bila kutaja kiwango cha asilimia kitakachopunguzwa.
Akizungumzia mshahara katika sekta binafsi, alisema kima cha chini hupangwa na bodi za mishahara za kisekta na kwamba majadiliano yalikuwepo ambayo yalipandishwa kutoka Sh 48,000 hadi Sh 700,000 kulingana na sekta.
Aidha alikitaka Chama cha Waajiri (ATE) kuliweka kwenye ajenda suala la waajiri wanaolipa chini ya kiwango watakapokwenda kukutana naye.
Alisema katika kipindi cha uongozi wake aliahidi ajira milioni moja lakini hadi anaondoka madarakani zaidi ya ajira milioni 2.6 zinapatikana kutoka serikalini pamoja na sekta binafsi.
Kikwete alionya baadhi ya waajiri ambao hawalipi viwango vilivyokubaliwa vya mishahara, kwa kusema hilo sio jambo la kiungwana na linahuzunisha.
“Waajiri hufikia makubaliano ya bodi za kisekta katika ulipaji wa mshahara.Tusikubali watu hawa waendelee kuhujumu haki za wafanyakazi.
“Naomba mamlaka husika tusikubali watu hawa wakaendelea kudhulumu haki za wafanyakazi,” alisema Rais Kikwete.
“Waajiri hufikia makubaliano ya bodi za kisekta katika ulipaji wa mshahara.Tusikubali watu hawa waendelee kuhujumu haki za wafanyakazi.
“Naomba mamlaka husika tusikubali watu hawa wakaendelea kudhulumu haki za wafanyakazi,” alisema Rais Kikwete.
Pia alisema wanajishughulisha kwa kadiri ya uwezo wao kutafuta matatizo yanayowakabili wafanyakazi, yale ambayo hayakupatiwa ufumbuzi si kwa sababu ya udogo wa dhamira bali ugumu wa tatizo lenyewe.
“Ambayo sijasema leo naendelea na nitaendelea kuyashughulikia mpaka nitakapokabidhi kwa huyo atakayekuja. Tutaendelea na Wizara ya Kazi na Ajira na ofisi ya takwimu kukuza ajira Tanzania,” alisema.
Alisisitiza kuwa rais ajaye atamkabidhi orodha ya yale mambo ambayo ni kiporo na anayojua mwenyewe na atatoa ushirikiano kwa rais ajaye.
Katika sherehe hizo Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Nicholus Mgaya alitaja madai waliyoyatoa kwa rais, kuwa makato ya kodi ni makubwa.
Mgaya alisema mwaka jana PAYE ilipungua hadi kufikia asilimia 12, lakini mategemeo yao ifikie asilimia 9 mwaka huu. Mgaya aliwataka wafanyakazi kutumia kura yao ipasavyo katika uchaguzi mkuu kwa kuchagua viongozi wanaojali tabaka la wafanyakazi.
No comments:
Post a Comment
TUNAOMBA MAONI YAKO JUU YA HII HABARI HAPA CHINI