Shughuli mbalimbali jijini Arusha jana zilisimama kwa muda wakati umati wa watu ulipofurika kumlaki Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyewasili mkoani hapa kwa ajili ya kuendesha harambee ya ujenzi wa Msikiti wa Patandi ulioko wilayani Arumeru. Lowassa, ambaye jana aliweka bayana kuwa atatangaza rasmi nia yake ya kuwania urais kwa tiketi ya CCM, alienda kuendesha harambee kwenye msikiti huo baada ya kutumwa kumwakilisha Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal.
Katika shughuli hiyo ya harambee, Lowassa alifanikiwa kuchangisha Sh235 milioni, ikiwa ni zaidi ya makisio ya msikiti huo ya kukusanya Sh200 milioni.
Harambee zimekuwa zikichukuliwa kama uwanja wa kampeni wa makada wanaowania urais kupitia chama tawala cha CCM na tangu apewe adhabu na wanachama wengine watano, Lowassa hakuwahi kuonekana kwenye uchangishaji fedha hadi wiki mbili zilizopita alipoalikwa na wagombea wengine wa urais wa CCM kwenye hafla iliyofanyika Zanzibar.
Jana, mbunge huyo wa Monduli alipokelewa kwa mbwembwe kwenye Uwanja wa Ndege wa Arusha ambako alilakiwa na umati wa watu, wakiwepo waendesha pikipiki ambao waliongoza msafara hadi viwanja vya msikiti mkuu wa Arusha.
Lowassa alifanya kazi hiyo ya harambee ya kuchangia mradi wa ujenzi wa jengo la ghorofa tano la msikiti huo litakalokuwa na shule ya sekondari, msikiti na kituo cha watoto yatima.
Barabara ya Uhuru, ambayo msafara huo ulipita ukiongozwa na pikipiki za polisi, ilifungwa na wafuasi wa Lowassa, ambao magari yao yalikuwa na nembo za ‘Team Lowassa’ na ‘Lowassa FU’ huku, wengine wakiwa na magari binafsi na waendesha pikipiki.
Lowassa alitua uwanja mdogo wa Arusha saa 7:30 mchana na alifika viwanja vya msikiti mkuu, saa 8:35 mchana na kulifanyika harambee ya kuchangia kituo cha elimu cha kiislam na msikiti wa Patandi na kupokelewa na umati huku wakiimba “rais, rais, rais” na kupokelewa na sheikh wa mkoa wa Arusha, Sheikh Shaaban Juma.
Katika msafara huo, Lowassa aliambatana na kaimu mkuu wa mkoa, Christopha Kangoye, mkuu wa wilaya ya Arumeru, Hasna Mwilima, mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba na mbunge wa viti maalum (CCM) mkoa wa Arusha, Namelock Sokoine.
Pia walikuwepo baadhi ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) wa wilaya, wafanyabiashara wakubwa wa mkoa wa Arusha, Mwanza na Kilimanjaro, sambamba na watu kadhaa wanaotarajiwa kugombea ubunge katika majimbo ya Arusha mjini, Arumeru Mashariki, Arumeru Magharibi, Monduli, Londigo na Ngorongoro.
Amshukuru Dk Bilal
Akizungumza katika harambee hiyo, Lowassa alisema si jambo dogo kupewa fursa kumwakilisha makamu wa Rais Dk Bilal katika hafla hiyo.
“Baada ya Makamu wa Rais kuniomba kuja kumwakilisha hapa, nilisita kidogo kwanza kutokana na kuwa hapa ni nyumbani, pia bado nipo kifungoni na pia nimekuwa nikialikwa katika harambee kadhaa za misikiti mkoani hapa na kushindwa kufika,” alisema ambaye amefungiwa kujihusiaha na shughuli za uchaguzi pamoja na makada wengine watano.
Alisema hata hivyo, baadaye alikubali kwa kutambua jambo ambalo anamwakilisha Makamu wa Rais ni la maendeleo kwa wananchi wa mkoa mzima wa Arusha na Taifa.
Avunja ukimya
Lowassa akizungumza na mamia ya watu waliohudhuria katika hafla hiyo, alisema amekuja Arusha akiwa na taarifa njema kuwa, Mei 24 atazungumza neno kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Aliwataka wakazi wa Arusha kumuunga mkono, siku hiyo kwa kujitokeza kwa wingi kumsikiliza.
“Mei 24 nitatoa neno siku hiyo na mtu akikuuliza unakwenda wapi mjibu nakwenda kwenye safari ya matumaini,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na umati wa watu.
Lowassa alipongeza wakazi wa Arusha kwa umoja wao, wanaoendelea kuuonyesha bila kujali itikadi zao, dini wala rangi, kutokana na kuhudhuria kwa wingi katika harambee hiyo.
“Hii ndio Arusha ninayoijua mimi, tumeishi kwa upendo na amani miaka mingi, tusikubali kugawanywa kwani sote ni binadamu tulio sawa,”alisema
Achangisha 235 milioni
Katika harambee hiyo, zaidi ya Sh235 milioni zilichangwa, wakati Lowassa, Makamu wa Rais na marafiki zake, walichanga Sh105 milioni.
Lowassa alikabidhi Sh50 milioni taslimu kwa sheikh wa mkoa wa Arusha, ikiwa ni mchango wake, makamu wa Rais na marafiki zake huku na kuahidi Sh50500 milioni.
Katika harambee, hiyo Sheikh wa mkoa, alijisahau na kumuita Lowassa ‘Mh Rais’, na kusababisha umati wa watu kushangilia. Fedha nyingine Sh130 milioni zilichangwa.
Baadhi ya wachangiaji walikuwa ni marafiki wa Lowassa walioongozwa na Mathias Manga, ambaye ni mjumbe wa NEC wa wilaya ya Arumeru, ambao walitoa Sh20milioni, Hussein Gonga Sh7 milioni na Mkandarasi Jeremiah Ayo alitoa Sh5milioni.
Mgombea watarajiwa wa ubunge, Mustapha Panju alitoa Sh6 milioni, Sioyi Sumari (Sh7 milioni), Kim Fute (Sh3 milioni), Philemon Mollel (Sh5 milioni), mbunge Peter Serukamba (Sh3 milioni) na mjumbe wa NEC kutoka jimbo la Busega, Dk Raphael Chegeni alichanga Sh1 milioni sawa na mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Namelock Sokoine.
Gharama
Awali akizungumza kabla ya kuanza kwa harambee hiyo, katibu wa Bakwata mkoani Arusha, Juma Masoud alisema kuwa mradi wa ujenzi wa msikiti huo unatarajiwa kugharimu Sh1 bilioni hadi kukamilika.
Alisema kuwa mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa ambayo wanatarajia kuitekeleza na kwamba ujenzi utahusisha ghorofa tano na ndani yake kutakuwa na kituo cha watoto yatima.
“Waumini katika msikiti huu kwa sasa wanakbiliwa na changamoto ya sehemu ya kufanyia ibada hivyo kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuokoa tatizo hilo,” alisema.
Alisisitzia kuwa awamu ya kwanza ya mradi huo unataraji kugharimu jumla ya kiasi cha Sh200 milioni na alimpongeza Lowassa kwa kujitoa katika juhudi za kusaidia maendeleo ndani ya jamii.
Naye Sheikh Shaaban alisema harambee hiyo inahusu wakazi wote wa Arusha kwani sekondari itakayojengwa haitakuwa ya dini moja hivyo, aliwashukuru wote waliochangia na mungu atawalipa.
Bomba.Com
No comments:
Post a Comment
TUNAOMBA MAONI YAKO JUU YA HII HABARI HAPA CHINI